Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za
binadamu yameitaka serikali ya Uganda kumkamata Rais Omar al-Bashir wa
Sudan na kumkabidhi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kwa tuhuma
za mauaji ya kimbari katika eneo la Darfur na jinai dhidi ya binadamu.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International
na Human Rights Watch yameitaka serikali ya Uganda kutekeleza wajibu
wake wa kimataifa na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC, Rais wa Sudan
ambaye alienda mjini Kampala kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais Yoweri
Museveni.
Muthoni Wanyeki, Mkurugenzi wa Amnesty International katika kanda ya
Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na eneo la Maziwa Makuu amesema Uganda
ni mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya
Jinai ICC na hivyo, iwapo itafeli kumkabidhi Rais wa Sudan, itakuwa
imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kimataifa. Hii ni katika hali
ambayo, baada ya kula kiapo hapo jana, Rais Museveni aliikashifu ICC na
kusema kuwa mahakama hiyo imegeuka na kuwa chombo cha kuwadhalilisha
viongozi wa Kiafrika huku ikiwasaza viongozi makatili wa nchi za
Magharibi
. Kauli ya Museveni iliwaghadhabisha wajumbe wa Marekani na
Umoja wa Ulaya waliokuwa wamehudhuria sherehe za kuapishwa kwake katika
Viwanja vya Kololo jijini Kampala na kuwafanya kuondoka kwenye hafla
hiyo.
Itakumbukwa kuwa, serikali ya Afrika Kusini ilikataa kumkamata Rais
Omar al-Bashir ambaye alishiriki mkutano wa viongozi wa Afrika
uliofanyika mjini Johannesburg Julai mwaka jana.
Aidha Kenya ilipuuza
wito wa kumkamata na kumkabidhi kiongozi huyo kwa Mahakama ya Kimataifa
ya Makosa ya Jinai ICC anakotakiwa kujibu tuhuma za mauaji ya kimbari
katika eneo la Darfur na jinai dhidi ya binadamu; alipohudhuria sherehe
za kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki mwaka
2013.
No comments:
Post a Comment