Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limefanya Operesheni na
Msako mkali katika Wilaya zake zote na kukamata makosa mbalimbali. Operesheni
hiyo ilianza kufanyika tarehe 22/02/2016 hadi 06/03/2016.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msadizi wa Polisi LAZARO MAMBOSASA – ACP amesema
katika Operesheni hiyo jumla ya silaha haramu 19 aina ya Gobore zimesalimishwa na silaha saba (7) zimekamatwa za watu waliokaidi utii wa sheria, mitambo
miwili ya kutengeneze silaha hizo haramu imekamatwa pamoja na watuhumiwa saba.
Kamanda MAMBOSASA amesema watuhumiwa wote ni wakazi wa
kijiji cha MANDA Tarafa ya MPWAYUNGU Wilaya ya Chamwino Mkoa wa Dodoma na wamekuwa wakimiliki silaha hizo kinyume cha
sheria na wakizitumia katika uhalifu
mbalimbali hasa uwindaji haramu katika hifadhi ya RUAHA inayopakana na mkoa wa
Iringa.
Aidha Kamanda MAMBOSASA amesema kutokana na operesheni hiyo
watu 19 waliweza kusalimisha silaha zao katika ofisi za serikali za vijiji na
hawakuchukuliwa hatua kwa kuwa walitii sheria bila shuruti.
Vilevile Kamanda MAMBOSASA amesema katika Wilaya za Dodoma,
Kondoa na Kongwa walikamatwa watuhumiwa 32 wa makosa ya Kupatikana na Bhangi,
jumla ya misokoto misokoto 672 ilikamatwa.
Watuhumiwa 11 walikamatwa kwa kosa la Kupatina na Pombe haramu ya Moshi
na jumla ya lita 260 zilikamatwa.
Watuhumiwa 7 walikamatwa kwa kosa la Kupatikana na madawa ya kulevya
aina ya Mirungi Kilogram 43.
Pia Operesheni ilihusisha makosa ya Usalama barabarani na
kukamatwa kwa jumla ya pikipiki 265 kwa makosa mbalimbali, ambapo pikipiki 241
zilitozwa faini na kiasi cha fedha Tsh. 7,230,000/= zilipatikana kutokana na
tozo.
Kamanda MAMBOSASA ametoa wito kuwa msako mkali unaendelea
na watu wote wanaomiliki silaha haramu kinyume cha Sheria wasalimishe silaha
hizo kwa hiari kwenye Ofisi za Serikali
na vituo vya Polisi mapema iwezekanavyo na hawatachukuliwa hatua. Wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha
Sheria wasiotayari kusalimisha wafichuliwe ili wachukuliwe hatua za kisheria
dhidi ya umiliki haramu wa silaha. Aidha wananchi waache kujihusisha na vitendo
vya uhalifu wa aina yoyote na kufanya kazi halali kujipatia kipato halali kwa
familia zao kwani msako utakuwa endelevu wasije wakaishia jela na kuziacha
familia zao zikiteseka.
Katika matukio mengine Kamanda
MAMBOSASA amesema mnamo tarehe 07.03.2016 majira ya saa 16:00 huko katika
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la BASILI MSABILA
mwenye miaka 24, Mwanafunzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa - HOMBOLO Dodoma
ngazi ya cheti, alifariki dunia wakati anatibiwa baada ya kujeruhiwa kichwani
kwa chuma na Mwanafunzi mwenzake aitwaye CHARLES MAKELE, miaka 19, mwenye miaka
19 mwanafunzi ngazi ya cheti kozi ya utawala chuo cha TAMISEMI Hombolo.
Uchunguzi wa awali
unaonesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kugombania chaja ya simu mali
ya marehemu, katika chumba cha bweni lao wanaishi wanafunzi wanne ambapo siku
ya tarehe 6/03/2016 hakukuwa na umeme na uliporudi umeme wanafunzi hao walianza
kugombani chaja hiyo ya simu ugomvi uliopelekea kuanza kupigana na ndipo BASILI MSABILA kujeruhiwa kwa chuma
chenye ncha kali kichwani na kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu
na kufariki dunia akiwa kwenye matibabu siku iliyofuata. Mtuhumiwa amekamatwa
na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unendelea.
Vilevile Kamanda
MAMBOSASA amesema tukio lingine limetokea tarehe 07.03.2016 majira ya saa
21:00hrs huko eneo la Kisasa Manispaa ya Dodoma ambapo mtu mmoja mwanaume
asiyefahamika jina mwenye umri kati ya miaka 23-25 aliuwawa kwa kukatwa na kitu
chenye ncha kali shingoni na mtu/watu waliojichukulia sheria mkononi kwa tuhuma
za kujaribu kuvunja dirisha la nyumba akiwa na wenzake waliofanikiwa kukimbia.
Uchunguzi unaendelea na Juhudi za kuwatafuta watu waliohusika na mauaji hayo
zinafanyika.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Dodoma LAZARO MAMBOSASA – ACP ametoawito kwa wananchi wa Dodoma
kutojichukulia sheria mkononi na kutofanya mauaji ya kikatili dhidi ya watu kwa
tuhuma nyepesi kwa kisingizio cha watu wenye hasira kali. Vitendo hivi
havitavumilika na sheria zifuatwe kila mtu ana haki ya kuishi na kujitetea
mbele ya sheria.
RPC Dodoma LAZARO MAMBOSASA - ACP akionyesha mitambo ya kutengenezea bunduki hizo.
RPC Dodoma LAZARO MAMBOSASA - ACP akionyesha mtambo wa kutengeneza bunduki haramu.
RPC Dodoma LAZARO MAMBOSASA - ACP akionyesha silaha aina ya gobore zilizokamatwa katika msako huo.
Kamanda wa Polisi Dodoma LAZARO MAMBOSASA akionyesha goroli zitumikazo katika magobore hayo.
RPC Dodoma Kamishna Msaidizi wa Polisi LAZARO MAMBOSASA - ACP
No comments:
Post a Comment